Huku Shirika la Ustawishaji Kilimo nchini, ADC likiadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, viongozi pamoja na wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo nchini wanaendeleza mbinu ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Viongozi hao wanatumia mbinu ya kilimo hifadhi ili kuepuka hasara msimu huu ambapo hali ya anga imebadilika kupita kiasi.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo mjini Kitale, Mkurugenzi Mkuu wa ADC Wilson Tonui amesisitiza kuwa msimu huu, hali ya anga imebadilika na hivyo kuwaomba wakulima kutumia mbinu tofauti ya ukulima msimu huu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande wake, afisa wa kilimo Laban Kiplagat amesema kuwa serikali imewapatia wakulima mbolea kwa bei nafuu itakayoboresha kilimo.
Baadhi ya wadau, wakiongozwa na mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya mbegu ya Kenya Seed Purity Ngirici, wamesema kuwa tangu kuanzishwa kwake, shirika hilo limeboresha kilimo kwa kuwafunza wakulima mbinu za kisasa za kilimo.