Kaunti ya Homa Bay ndiyo mwenyeji wa sherehe za Madaraka mwaka huu, zitakazoandaliwa katika uwanja wa Raila Odinga.
Hayo yalitangazwa leo Alhamisi na katibu katika wizara ya usalama wa taifa Dkt. Raymond Omollo, aliyeongoza ujumbe wa ngazi za juu serikalini kukagua shughuli za maandalizi.
“Sherehe za mwaka huu za Madaraka, zitaandaliwa katika kaunti ya Homa Bay, katika uwanja wa Raila Odinga,” alisema Dkt. Omollo kupitia ukurasa wa X.
Kulingana na katibu huyo, maudhui ya sherehe hizo ni “Ustawi wa uchumi wa baharini na shughuli za majini”.
Dkt.Omollo alisema maandalizi ya sherehe hizo yanaendelea vyema na yatakamilika kwa wakati.
“Maandalizi ya sherehe hizo yameshika kasi, ili kuonyesha uwezo muhimu wa eneo la Nyanza Kusini,” aliongeza katibu huyo.
Katika ziara hiyo, Dkt. Omollo aliandamana na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, katibu katika idara ya barabara Mhandisi John Mbugua, mwenzake wa uchukuzi Mohamed Daghar na mbunge wa Homa Bay mjini Peter Kaluma.