Mwanamuziki wa Uganda Sheebah Karungi amerejea nchini humo kutoka Canada ambapo amekaa kwa miezi kadhaa.
Karungi ambaye pia anafahamika kama Queen Karma aliondoka Uganda Oktoba mwaka jana muda mfupi baada ya tamasha lake katika uwanja wa Lugogo ambalo lilihudhuriwa na watu wengi.
Akiwa Canada, Sheebah alijifungua mtoto wa kiume kwa jina Amir mwezi Novemba mwaka jana. Inaarifiwa kwamba uamuzi wa kwenda kujifungua nchini Canada ulichochewa na haja ya mtoto huyo kuwa na uraia wa huko.
Sheebah alitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe jana ambapo alipokelewa na watu wake wa karibu.
Muda mfupi baada ya kuondoka mwaka jana, rafiki yake wa karibu ambaye ni mcheza densi Ritah Danchall alihojiwa na kufichua kwamba Sheebah angekaa ughaibuni kwa zaidi ya miezi sita.
Rita ambaye ana ukaribu wa pekee na Sheebah alilalamika kwamba angemkosa sana kwa kipindi hicho ambacho angekuwa nje. Alielezea kwamba yeye huwa mpweke katika tasnia ya muziki na burudani nchini Uganda na Sheebah pekee ndiye humsikiliza wakati ana shida.