Watu wasiopungua tisa wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya shambulizi la ndege isiyo na rubani ya Urusi kulenga basi lililokuwa likisafirisha wafanyakazi katika eneo la Dnipropetrovsk, Ukraine, Gavana Sergiy Lysak alithibitisha.
Shambulizi la adui limeangamiza maisha ya watu tisa” katika jiji la Marganets, kusini mashariki mwa Ukraine, aliandika Lysak kupitia Telegram.
Ameongeza kuwa “idadi ya majeruhi inaendelea kuongezeka” na kufika 30.
Mamlaka za Ukraine pia zimeripoti milipuko na moto maeneo ya Kyiv, Kharkiv, Poltava, Odesa na Belgorod usiku kucha baada ya mashambulizi mengine ya Urusi.
Mashambulizi haya yametokea wakati wajumbe kutoka Marekani, Ukraine, na mataifa ya Ulaya wakijiandaa kwa duru mpya ya mazungumzo nchini Uingereza siku ya Jumatano, yenye lengo la kumaliza mzozo huu uliodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.