Wanajeshi wanne wameuawa na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa katika shambulio la ndege isiyo na rubani lililoilenga kambi ya jeshi kaskazini mwa Israel, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema.
IDF liliongeza kuwa wanajeshi saba wamejeruhiwa vibaya katika shambulio hilo kwenye kambi “karibu na Binyamina” – mji ulioko umbali wa maili 20 (33km) kusini mwa Haifa.
Hezbollah imedai kuhusika na shambulio hilo ambalo ilisema liliilenga kambi ya mafunzo ya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) Brigedi ya Golani katika eneo hilo lenye makao yake makuu kati ya Tel Aviv na Haifa.
Ofisi ya vyombo vya habari vya kundi hilo lenye silaha imesema kuwa shambulio hilo lilikuwa ni kujibu mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon na Beirut siku ya Alhamisi.
Kundi hilo limesema lililenga kambi hiyo kaskazini mwa Israel kwa kutumia “kundi la ndege zisizo na rubani”.