Shambulizi la bomu latibuliwa Uganda

Watu wawili wanaoshukiwa kuwa magaidi na waliokuwa wamejihami kwa mabomu waliuawa.

Marion Bosire
1 Min Read

Maafisa wa jeshi nchini Uganda wamesema kwamba wametibua kile kinachoaminika kuwa shambulizi la bomu, la washambulizi wa kujitoa mhanga kufa.

Kaimu msemaji wa jeshi nchini humo Chris Magezi alitoa taarifa kuhusu tukio hilo akisema kwamba maafisa wa kitengo cha jeshi la nchi hiyo cha kukabiliana na ugaidi kilifanikiwa kutibua njama ya washambuliaji wawili.

Wawili hao wanadaiwa kulenga eneo la Munyonyo ambako hafla ya siku kuu ya wafia dini inaandaliwa wakiwa wamejihami kwa mabomu.

Kulingana na Magezi, maafisa hao wa jeshi walikuwa wamepokea taarifa za ujasusi kabla ya kuvizia wawili hao na kufanikiwa kuwaua huku wakiharibu mabomu waliyokuwa nayo.

“Kikosi cha kukabiliana na ugaidi asubuhi ya leo kilivizia na kuua magaidi wawili waliokuwa wamejihami katika eneo la Munyonyo,” alisemaMagezi katika taarifa.

Aliongeza kusema kwamba maafisa wa usalama waliongeza doria katika eneo husika ili kuhakikisha maadhimisho ya siku ya wafia dini yanaendelea bila matatizo.

Magezi aliwataka wananchi kusalia watulivu lakini wawe macho na kuripoti watu wanaowashuku kwa maafisa wa usalama ili hatua zichukuliwe.

Share This Article