SHA: Serikali haina deni la shilingi bilioni 30 kwa hospitali za kibinafsi

Tom Mathinji
2 Min Read
Wakenya kupata huduma za SHA bila masharti katika vituo vya afya vya umma.

Halmashauri ya Afya ya Jamii SHA, imepuuzilia mbali madai kwamba inadaiwa na hospitali za mashinani na mijini za kibinafsi (RUPHA) shilingi bilioni 30, jinsi ilivyoripotiwa awali.

Kupitia kwa taarifa, SHA badala yake ilisema hospitali hizo zitapokea mafunzo kabambe kuhusu usimamizi wa malipo ili kuboresha uwasilishaji wa fomu za kudai malipo kwa lengo la kuzuia ucheleweshaji.

“Tungependa kuthibitisha kuwa serikali haina deni la shilingi bilioni 30 kwa RUPHA jinsi ilivyoripotiwa. Taasisi za afya za RUPHA,  zitapokea mafunzo kuhusu usimamizi wa ulipaji, ili kuzuia ucheleweshaji,” ilisema SHA kwenye taarifa.

SHA ilisema serikali imejitolea kutoa huduma za afya ya msingi katika vituo vyote vya afya vya serikali kote nchini, huku ikijizatiti kukamilisha ulipaji wa deni wa iliyokuwa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya  (NHIF).

Hadi kufikia sasa, SHA ilisema imelipa shilingi bilioni 10 kati ya bilioni 19 inazodaiwa na NHIF.

“SHA inashirikiana na vituo vya afya kukamilisha ulipaji deni la NHIF, ambapo hadi sasa, asilimia 60 ya deni hilo limelipwa,” iliongeza SHA.

Halmashauri hiyo iliwahakikishia Wakenya wote waliosajiliwa na SHA, kuwa watapokea matibabu katika vituo vyote vya afya bila vizuizi vyovyote.

Aidha, SHA  ilidokeza kuwa imelipa shilingi bilioni 5.1 wiki hii, huku idadi jumla ya malipo yaliyotolewa tangu mwezi Oktoba mwaka 2024 yakiwa bilioni.18.29.

 

Share This Article