SHA kukutana na wadau kujadili bima ya saratani

Marion Bosire
2 Min Read
Dkt. Mercy Mwangangi, Afisa Mkuu Mtendaji wa SHA

Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA imesema kwamba inapanga kufanya mkutano wiki ijayo na wadau kujadili viwango vya bima kwa wanaougua saratani.

Katika taarifa iliyotiwa saini na Afisa Mkuu Mtendaji wa SHA Dkt. Mercy Mwangangi, mamlaka hiyo imeelezea kwamba imejitolea kuhakikisha kila Mkenya anapata huduma bora na nafuu za afya zikiwemo za matibabu ya saratani.

Dkt. Mwangangi alisema kwenye taarifa hiyo kwamba wamepokea malalamishi kutoka kwa wateja kadhaa kuhusu viwango vya malipo yanayotolewa na SHA kwa matibabu ya saratani.

“Lengo letu ni kuhakikisha Wakenya wanapokea huduma wanazohitaji bila mzigo mkubwa wa kifedha,” aliongeza Afisa Mkuu Mtendaji huyo katika taarifa yake akitambua kwamba wamepokea mapendekezo na malalamisji kutoka kwa mtandao wa mashirika yanayohusiana na matibabu ya saratani nchini -KENCO.

Ametetea viwango vya sasa vya malipo ya matibabu ya saratani vinavyotolewa na SHA akisema viliafikiwa kupitia utathmini wa ushahidi uliopo.

Licha ya utetezi huo, aliashiria kuwa watajadiliana na wawakilishi wa KENCO wiki ijayo ili kuibuka na namna bora ya kuhudumia wateja wa saratani.

Aliongeza kwamba kwa sasa jopo linalohusika na kuweka viwango vya malipo kwa kila huduma linachunguza upya malipo ya saratani kwa lengo la kuyaongeza.

Kulingana na Mwangangi, kufikia sasa, SHA imeongeza malipo inayotoa kwa matibabu ya saratani kutoka shilingi 400,000 hadi shilingi 550,000.

Share This Article