SHA itafanikiwa, asema Rais Ruto huku Duale akitakiwa kujiuzulu

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto ameelezea imani yake kwamba Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA itafikia lengo lake la kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, almaarufu UHC.

Kupitia mamlaka hiyo, Ruto anasema Wakenya wote sasa wanapata huduma za matibabu bila kujali vyeo vyao katika jamii kama iliyokuwa awali.

“Huduma za afya kamwe si kitu ambacho watu wachache wanaweza wakamudu, lakini ni haki ya kila Mkenya. Pia tunaufanya mfumo wetu wa afya kuwa wa kidigitali ili kuziba mianya ambayo ilivuruga utenda kazi wa iliyokuwa Hazina ya Bima ya Afya ya Kitaifa, NHIF, ili kuhakikisha Mamlaka mpya ya Afya ya Jamii (SHA) inatimiza kusudio lake,” alisema Rais Ruto alipokutana na viongozi wa mashinani kutoka kaunti ya Kiambu katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatano.

“SHA lazima ifanye kazi, na itafanya kazi.”

Matamshi ya Rais Ruto yanakuja saa chache baada ya wabunge wanaoegemea mrengo wa Kenya Moja kumpa Waziri wa Afya Aden Duale makataa ya saa 48 kujiuzulu la sivyo wawasilishe hoja ya kumtimua kwenye wadhifa huo pale bunge litakaporejelea vikao vyake mwishoni mwa mwezi ujao.

Wakiongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, wabunge hao wamedai kuwa SHA imeghubikwa na wingu la ufisadi ambao umewafanya Wakenya ambao ni walipa kodi kupoteza mabilioni ya pesa.

Duale ameapa kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya SHA zinatumiwa kuhakikisha kila Mkenya anapata huduma bora za matibabu.

Tayari, Wizara ya Fedha imesitisha utoaji wa shilingi bilioni 10 kwa hospitali kadhaa zilizojiandikisha kutoa huduma za matibabu chini ya mamlaka hiyo kutokana na madai ya ufisadi.

Share This Article