Katika kile kinachoonekana kama hatua ya kupiga jeki ugatuzi, Serikali za kaunti zimetengewa shilingi bilioni 405.1 kwenye bajeti ya mwaka 2025/2026.
Akiwasilisha bajeti ya mwaka huu wa kifedha kwenye majengo ya bunge Alhamisi alasiri, waziri wa Fedha John Mbadi alisema mgao huo ni nyongeza ya asilimia 17.6 katika bajeti ya mwaka 2024/2025.
Kaunti ya Nairobi ndiyo iliyonufaika pakubwa kwa kutengewa shilingi Bilioni 21.1, ikifuatwa na Nakuru kwa shilingi Bilioni 14.3 Turkana shilingi bilioni 13.8 nayo Wajir ikirithika na shilingi bilioni 10.3.
Ilikufanikisha mpango wa elimu bila malipo, waziri Mbadi alitangaz kuwa elimu ya msingi bila malipo itapokea shilingi Bilioni 7.0, sekondari msingi ikipata shilingi Bilioni 28.9, huku shule za upili za kutwa zikifaidika na shilingi Bilioni 51.9.
Aidha Mbadi alitenga shilingi Bilioni 5.9 kwa kufanikisha mitihani ya kitaifa, shilingi Bilioni 3.0 za mpango wa lishe shuleni, huku uajiri wa walimu wanagenzi ukitengewa shilingi Bilioni 7.2 nazo Taasisi za kiufundi zikitengewa shilingi bilioni 4.0.
Maudhui ya bajeti ya mwaka huu ni ufufuzi endelevu wa kiuchumi kwa maisha bora,kubuni nafasi za ajira,ukuzi wa biashara na ustawi wa viwanda kuambatana na ajenda ya serikali ya mageuzi ya kiuchumi.