Serikali yazindua kadi maalum za afya kwa wasichana wadogo wanaojifungua

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Afya Aden Duale.

Kupitia mpango wa Afya kwa Wote UHC, wizara ya Afya imeanzisha kadi maalum za afya, zitakazotumiwa na wasichana wanaojifungua wakiwa na umri mdogo.

Kulingana na wizara hiyo, kadi hizo zitaondoa vizingiti vinavyowanyima wasichana hao kupata huduma muhimu za afya.

Kwenye taarifa kupitia ukurasa wa X leo Jumamosi, Waziri wa Afya Aden Duale alisema hatua hiyo inanuiwa kuhakikisha kina mama walio na umri mdogo ambao hukumbwa na unyanyapaa na kupuuzwa, wanapokea huduma za afya za kabla ya kujifungua, baada ya kujifungua, chanjo,mpango wa uzazi na ushauri nasaha.

“kwa kuwajumuisha rasmi kwenye mfumo wa afya, serikali inapunguza hatari ya mimba na idadi ya wasichana wanaoacha shule, huku pia ikishughulikia swala la umaskini,” alisema Duale.

Waziri huyo alisema kushirikisha mipango kama vile Linda Mama, kadi hizi ni ishara ya kutekeleza mfumo jumuishi wa afya ambapo kila mmoja hususana walio na umri mdogo wanajumuishwa mfumo wa huduma za afya.

TAGGED:
Share This Article