Rais William Ruto amezindua mpango wa fursa za uanagenzi katika mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu leo katika Ikulu ya Nairobi.
Kiongozi wa nchi alisema kwamba mpango huo unalenga kusuluhisha mahitaji yanayoonekana ya mradi wa nyumba za gharama nafuu na utawapa vijana wapatao elfu 4 fursa za ajira za muda katika kiwango cha uanagenzi.
Walengwa wa fursa hizo ni pamoja na waliosomea kozi zinazoambatana na ujenzi kama usanifu majengo, usoroveya, uhandisi, usimamizi wa ujenzi miongoni mwa nyingine, katika taasisi za mafunzo ya kiufundi.
Katika juhudi za kufanikisha mpango huo, Rais William Ruto alielezea kwamba serikali itaongeza kwa muda mfupi idadi ya kampuni za ushauri katika mradi wa nyumba za gharama nafuu.
Kampuni hizo zitaongezwa kutoka 39 hadi 70, ili ziweze kumudu idadi kubwa ya watu watakaopata ajira hizo za uanagenzi huku wafanyakazi jumla wa mradi huo wakitarajiwa kuongezeka kutoka elfu 320 wa sasa hadi laki 6.
Zamu za kazi pia zitaongezwa kutoka zamu moja hadi mbili kila siku ili kumudu idadi ya vijana watakaoajiriwa.
“Maelekezo yangu kwa wizara ya ardhi kwa ushirikiano na kampuni za ushauri ni kupanga upya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ili kuongeza idadi ya wanaofanya kazi huko kutoka 320,000 hadi 600,000” alisema rais Ruto.