Serikali imetambua wajibu muhimu ambao hutekelezwa na watumishi wa umma, waliotajwa kuwa nguzo kuu katika maendeleo ya taifa.
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, alisema watumishi wa umma hapa nchini, wamesaidia pakubwa taifa hili kupiga hatua, katika kuafikia malengo yake.
Akizungumza wakati wa kuwatuza watumishi wa umma 24 waliostafu kutoka kwa afisi ya Rais, Koskei alisema muhula wa kuhudumu wa watumishi hao wa umma ulijumuisha matukio mengi ya kihistoria, ukiwemo ule mfumo wa upigaji kura kutumia foleni, almaarufu mlolongo, kufanyiwa marekebisho kwa kifungu nambari 2A ya katiba ya Kenya, na kuzinduliwa kwa katiba mpya ya taifa hili mwaka 2010.
Koskei aliwahimiza watumishi wa umma waliostaafu kukumbatia ukurasa mpya wa maisha yao, akiwataka wajihusishe kama washauri na viongozi katika jamii zao, akiongeza kuwa hekima yao inasalia kuwa muhimu katika taifa hili.
“Hali ya kustaafu haipotezi thamani yako, lakini hukuza hekima yako,’ alisema Koskei.
Katika sherehe hiyo iliyoandaliwa katika Jumba la mikutano ya Kimataifa (KICC), familia za watumishi wa umma waliostaafu pia zilitambuliwa kwa jukumu kuu la kuwapiga jeki watumishi wa umma.
Sherehe hiyo ilikuwa sehemu ya mpango wa serikali wa kufanyia mabadiliko utumishi wa umma, kwa lengo la kutuza huduma hiyo na kuhifadhi kumbukumbu za kitaasisi.
Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma Amos Gathecha, ni miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo.