Serikali yatwaa ujenzi wa uwanja wa Isiolo

Baada ya ujenzi kusimama kwa muda wa miaka sita, serikali ya Kenya kupitia kwa wizara ya michezo, imejitwika jukumu la kujenga na kukamilisha uwanja wa Isiolo.

Dismas Otuke
2 Min Read

Uwanja wa Isiolo umeongezwa kwenye orodha ya viwanja ambavyo vinakarabatiwa humu nchini huku taifa hili likikaribia kuandaa mashindano mawili makubwa ya soka barani Afrika, mashindano ya soka kwa wachezaji wa nyumbani pekee CHAN mwezi Agosti na fainali za kombe la bara Afrika mwaka 2027.

Mashindano hayo mawili yataandaliwa na Kenya, kwa ushirikiano na mataifa ya Uganda na Tanzania.

Baada ya ujenzi kusimama kwa muda wa miaka sita, serikali ya Kenya kupitia kwa wizara ya michezo, imejitwika jukumu la kujenga na kukamilisha uwanja wa Isiolo.

Kufuatia ukaguzi uliofanywa Alhamisi mchana, waziri wa michezo Salim Mvurya, aliamurisha maafisa wa ‘Sports Kenya’ kuandaa michoro ya viwanja vya kisasa vya kimataifa katika muda wa majuma mawili.

Punde tuu mifano hiyo itakapowasilishwa, serikali itaanzisha rasmi ujenzi wa uwanja huo.

Maafisa wakuu serikalini waliokuwa wakati wa ukaguzi huo wakiwamo seneta wa Isiolo Fatuma Dullo, walifurahishwa na umauzi huo wakisema kuwa ujenzi wa uwanja wa Isiolo utafufua matumaini ya vijana wa eneo hilo hasa wale wenye ari ya kushiriki michezoni.

Na katika jitihada za kutambua na kukuza talanta za chipukizi humu nchini, zaidi ya viwanja 10 vinakarabatiwa katika taifa hili pamoja na kujengwa upya kwa uwanja wa Talanta City na serikali ya Kenya, mbali na shule za michezo 37 ambazo zitajengwa katika sehemu mbali mbali humu nchini.

Share This Article