Serikali yakana madai ya kuongeza karo ya shule za sekondari

Martin Mwanje
2 Min Read
Julius Ogamba - Waziri wa Elimu

Serikali imekanusha madai kuwa wazazi watalazimika kuwalipia watoto wao wanaosomea shule za sekondari za umma kitita cha shilingi 53,554 kama karo kwa mwaka kuanzia mwezi Januari mwakani. 

Waziri wa Elimu Julius Ogamba ametaja ripoti hizo zilizochapishwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa za uongo.

Kwenye taarifa, Ogamba amesisitiza kuwa karo katika shule za sekondari ya juu itasalia kuwa 22,244 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka.

“Nadhari yetu imevutiwa na ripoti katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa karo inayolipwa na wanafunzi katika shule za sekondari ya juu za umma imeongezwa,” Waziri Ogamba alielezea kugutushwa kwake.

“Wazazi, wanafunzi na umma kwa jumla wanataarifiwa kwamba hakujakuwa na ongezeko la karo ya malazi au karo yoyote ile inayolipwa na wanafunzi. Mwongozo uliopo kwa sasa kutoka kwa Wizara ya Elimu juu ya malipo ya karo ya shule za malazi utaendelea kutumiwa jinsi ambavyo imekuwa siku zilizopita.”

Waziri akihakikisha kuwa serikali itaendelea kuwajibika kama inavyohitajika kikatiba kugharimia elimu ya wanafunzi katika shule za sekondari ya juu.

Kulingana na Waziri, ada zilizoidhinishwa kwa kiwnago hiki cha elimu ni shilingi 22,244.

Ripoti za kuongezwa kwa karo ya shule za sekondari za umma zilikuwa zimewavunja moyo wazazi wengi ambao tayari wameelemewa na mzigo wa kugharimia maisha ya kila siku ya familia zao.

Share This Article