Serikali inachunguza madai ya uwepo wa wanajeshi wa Somalia nchini hususan katika kaunti ya Mandera, haya ni kulingana na waziri wa usalama wa taifa Kipchumba Murkomen.
Aliyasema hayo wakati wa kikao cha Jukwaa la Usalama huko Busia kufuatia ripoti kutoka kwa wakazi wa kaunti ya Mandera kwamba wanajeshi wa Jubbaland wamevuka mpaka kinyume cha sheria na kuingia humu nchini.
Akijibu maswali ya wanahabari, Waziri Murkomen alisema hakuna wanajeshi kama hao nchini na serikali haifahamu chochote kuhusu uwepo wao.
Murkomrn alisema wapo kuna watu wamevuka mpaka kufuatia mapigano kwenye nchi yao, serikali itawatambua na kuwachukulia hatua kulingana na sheria za kimataifa.
Waziri huyo alielezea kwamba jukumu la kwanza la serikali ni kuhakikisha kwamba hakuna wahalifu wanavuka mpaka na kuingia humu nchini.
Lakini wanaotafuta hifadhi alisema watasaidiwa kwa ushirikiano na seriali ya Somali ambayo kulingana naye ina uhusiano mwema na Kenya.
Uvumi kuhusu uwepo wa wanajeshi hao wa Jubbaland katika eneo bunge la Mandera Mashariki ulisababisha maandamano humo huku Gavana wa Mandera Mohammed Adan akithibitisha kwamba wapo.
Gavana Adan alihimiza serikali kuchukua hatua za haraka kuhusu suala hilo kabla mambo hayajaharibika.