Serikali imezindua mradi wa shilingi milioni 620 wa uunganishaji nguvu za umeme katika maeneo ya mashinani kaunti ya Nyamira, katika juhudi za kufanikisha shughuli za uchumi na biashara kwenye eneo hilo.
Kulingana na waziri wa Nishati Opiyo Wandayi, mradi huo unaotekelezwa na shirika la uunganishaji nguvu za umeme mashinani (REREC) ni muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme nafuu kwa wakazi na biashara katika maeneo ya mashinani kwenye kaunti hiyo.
“Idadi kubwa ya wakazi katika kaunti ya Nyamira, inapatikana katika maeneo ya mashinani na wakazi hao hawajapata fursa ya kunufaika na nguvu za umeme,” alisema Wandayi.
Waziri huyo alisema serikali imeweka mikakati ya kusambaza nguvu za umeme katika sehemu zote za mashinani.
“Tutahakikisha tunatekeleza jukumu hili bila mapendeleo, ili kuboresha maisha ya wale wanaoishi sehemu za mashinani,” alisema Wandayi.