Rais William Ruto ameficua mipango kadhaa inayolenga kusuluhisha tatizo sugu la ukosefu wa ajira kati ya vijana nchini.
Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya siku ya vijana ulimwenguni katika kaunti ya Kakamega, Ruto alisisitiza haja ya kuunda nafasi za kazi kwa haraka na njia ya kimkakati.
“Tatizo moja kubwa kati ya vijana ni ukosefu wa ajira na fursa” alisema Rais Ruto.
Kati ya mipango ambayo Rais amependekeza ni mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu unaotarajiwa kutoa fursa zaidi ya milioni moja za ajira ambapo nyumba 161,000 zinaendelea kujengwa.
Kufikia sasa mradi huo umeajiri watu wapatao 320,000 kiwango ambacho kinatarajiwa kuongezeka mara dufu katika miezi michache ijayo.
Serikali imeazinsha pia lango la mitandaoni kwa jina “Kuna Form” linalonuiwa kuunganisha vijana na fursa za biashara kwenye miradi ya serikali.
Rais Ruto aliangazia pia mpango wa ajira ughaibuni ambapo wakenya wapatao 420,000 wapata ajira katika mataifa ya nje katika muda wa miaka miwili unusu iliyopita.
Hatua nyingine iliyochukuliwa na serikali ni upanuzi wa mifumo ya kidijitali ambapo vijana milioni 1.9 wamepata ujuzi wa kidijitali huku laki 3 kati yao wakipata ajira za kidijitali.
Mipango mingine ni pamoja na Kandarasi Mtaani utakaotoa fursa laki 2 za ajira na uzinduzi ujao wa ufadhili wa biashara za vijana wa bilioni 9.75.
Kulingana na kiongozi wa nchi, mipango hii ni sehemu ya mpango mkuu wa kuwapa vijana ujuzi, fursa na usaidizi wanaohitaji kunawiri katika soko la ajira la karne ya 21.