Rais William Ruto amesema kwamba serikali imeanzisha mipango mbali mbali inayolenga kurejesha hadhi ya jiji la Nairobi kama jiji kuu la taifa hili.
Mipango hiyo ni pamoja na kutenga shilingi bilioni 2.1 za kuboresha muundomsingi wa barabara, ujenzi wa madarasa zaidi na utoaji wa maji ya kutosha kwa wakazi.
Akizungumza jana alipohudhuria ibada katika kanisa la AIC Kibra, Rais alisema pia kwamba juhudi za kusafisha mto Nairobi zinaendelea akifichua kwamba vijana elfu 30, zaidi watasajiliwa kujiunga na wale elfu 20 ambao wanaendeleza kazi hiyo.
Kiongozi wa nchi alilalamika kwamba asilimia 60 ya wakazi wa Nairobi wanaishi kwenye mitaa ya mabanda, suala alilosema litatatuliwa na ujenzi unaoendelea wa nyumba za gharama nafuu.
Rais Ruto alisema pia kwamba serikali itatenga shilingi milioni 500 mwaka ujao wa matumizi ya pesa za serikali zitakazotumiwa kulainisha uunganishaji wa stima katika mitaa ya mabanda.
Alisema lengo la mpango huo ni kushughulikia miunganisho duni ya stima ambayo huwa inasababisha visa vya moto ambao huharibu makazi, mali na hata kusababisha vifo.
Mpango huo kulingana na Rais utahakikishia wakazi usalama na kulinda maisha yao pamoja na mali. Rais alikutana na waathiriwa wa kisa cha hivi maajuzi cha moto Kibra ambapo alitoa msaada wa chakula na magodoro.