Serikali ya Nairobi yaagizwa kuondoa taka mbele ya ofisi za Kenya Power

Martin Mwanje
2 Min Read

Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) imeiagiza serikali ya kaunti ya Nairobi kuondoa rundo la taka ilizomwaga mbele ya ofisi za kampuni ya Kenya Power mara moja.

Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa utekelezaji sheria wa mamlaka hiyo Dkt. Ayub Macharia,

NEMA inasema hatua hiyo ilikuwa ukiukaji wa sheria na ni hatari kwa afya ya wakazi wa eneo hilo.

Dkt. Macharia ameonya kuwa mamlaka hiyo itachukua hatua za kisheria dhidi ya serikali ya Gavana Johnson Sakaja ikiwa itashindwa kutii agizo hilo.

Jana Jumatatu, kulikuwa na kizaazaa nje ya makao makuu ya kampuni ya Kenya Power katika jumba la Stima Plaza katikati ya jijini kuu la Nairobi.

Hii ni baada ya wafanyakazi wa kuzoa taka kutoka kaunti ya Nairobi kumwaga taka nje ya lango ya jumba hilo.

Tukio hilo liliathiri utoaji huduma kwa kipindi kirefu huku wafanyakazi wa Kenya Power na waliofika kutafuta huduma wakilazimika kuvumilia uvundo wa taka.

Kulingana na Meneja wa bishara katika kampuni ya Kenya Power Mhandisi Rosemary Oduor, kaunti ya Nairobi ilikuwa ikilipiza kisasi baada ya Kenya Power kukata umeme katika jumba la City Hall Ijumaa iliyopita kutokana na deni la shilingi bilioni tatu ambazo kaunti inadaiwa.

Hata hivyo, kaunti ya Nairobi imesema kuwa ilirejesha umeme Ijumaa iliyopita na mazungumzo yamekuwa yakiendelea kwa miaka miwili iliyopita, kaunti ikiahidi kulipa deni.

Serikali ya kaunti ya Nairobi kwa upande wake inasema deni inalodai Kenya Power ni kubwa zaidi kuliko wanalodaiwa na kampuni hiyo ya umeme.

 

Share This Article