Serikali ya Kenya imetafuta nafasi za ajira laki mbili kwa Wakenya ughaibuni tangu Juni mwaka jana katika hatua hiyo imepunguza pakubwa mzigo wa ukosefu wa ajira nchini, kulingana na Katibu wa Wizara ya Leba, Shadrack Mwadime.
Mwadime ameongeza kuwa serikali inalenga kubuni nafasi za ajira milioni 1 kila mwaka kwa Wakenya kufanya kazi ughaibuni, ili kupunguza idadi ya wasio na ajira nchini kutoka kiwango cha sasa cha watu milioni 5.
Akizungumza leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA, alipowaaga Wakenya 20 wanaoelekea Abu Dhabi kufanya kazi za teksi, Mwadime amesema serikali inapania kupanua nafasi za ajira kwa vijana wa humu nchini.
“Tunaambiwa kuna vijana milioni 5 wasio na kazi na jukumu letu ni kutafuta nafasi nyingi za ajira iwekezekanavyo,” alisema Mwadime.

Katibu huyo ameongeza kuwa kazi za ughaibuni pia zinawezesha kuongeza teknolojia ya utendakazi pamoja na kuimarisha uchumi wa Kenya.
“Tunachofanya kitasaidia kuleta maarifa na teknolojia mpya za utendakazi kutokana na tajiriba watakayopata ughaibuni.”
Mwadime amesisitiza kuwa serikali inawekeza katika kubuni nafasi za ajira zaidi ikilenga mataifa ya Magharibi ya Ulaya, Ghuba, na masoko mengine ibuka ya ajira na kuwataka Wakenya kukumbatia fursa zilizopo kupunguza ukosefu wa ajira.