Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen,amesema serikali imeanzisha mafunzo ya dharura kwa machifu na manaibu wao 8,102 huku kundi la kwanza la maafisa elfu-1 likiendelea kupokea mafunzo wakati huu.
Akiongea katika Chuo cha Taifa cha Polisi wa Utawala eneo la Embakasi wakati wa ufunguzi wa kozi ya mafunzo ya kisheria na usimamizi wa usalama kwa Machifu na Manaibu wao, waziri alisema serikali pia itazindua taratibu za utendakazi ili kutoa mwongozo kuhusu mahusiano ya maafisa wa utawala wa serikali ya taifa na wale wa kitengo cha polisi wa utawala wa serikali kuu.
“Tumeanzisha mpango wa utoaji mafunzo kwa Machifu na Manaibu wao, kundi la kwanza likiwa na maafisa hao 1,000,” alidokeza waziri huyo.
Murkomen wakati huo huo, alitangaza kwamba Machifu pamoja na Manaibu wao kwenye maeneo ambako usalama umedorora watapokea mafunzo ya kijeshi ili kuhakikisha jamii zinaoishi humo zina uthabiti, uhalifu unazuiwa na maendeleo kunawiri.
“Mara ya mwisho Machifu na Manaibu wao walipata mafunzo ilikuwa mwaka 2018, na hata wakati huo wengine walikosa mafunzo hayo. Wengine hawajapewa mafunzo kwa muda wa miaka 25,” alisema Murkomen.
Waziri alisema kuwa katika siku za usoni, serikali itaanza kuwasilisha sare rasmi za Machifu na Manibu wao kwenye Makao Makuu ya kaunti ili wazichukue.
Kwa sasa machifu huchukua sare zao rasmi katika chuo cha mafunzo ya polisi wa utawala jijini Nairobi.