Serikali kutekeleza maendeleo jumuishi kote nchini

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amesisitiza dhamira ya utawala wake ya kuleta maendeleo jumuishi kote nchini.

Akizungumza wakati wa ziara ya kimaendeleo katika mji wa Masalani, Kaunti Ndogo ya Ijara, Kaunti ya Garissa, Rais alihakikishia wakazi kwamba maeneo ya Kaskazini mwa Kenya yatapatiwa kipaumbele sawa katika mipango ya maendeleo ya taifa.

Kiongozi wa nchi alisisitiza kwamba serikali yake inawekeza pakubwa katika miundombinu ya barabara, uunganishaji umeme, makazi nafuu, masoko ya kisasa na miradi mingine muhimu inayolenga kuinua jamii zote.

Rais alibainisha kuwa kwa miaka mingi, eneo la Kaskazini mwa Kenya limekuwa likichukuliwa kimakosa kuwa eneo lisilo na uwezo mkubwa wa maendeleo, dhana ambayo alisema serikali yake imejizatiti kubadilisha kupitia uwekezaji wa mabadiliko makubwa.

Alisema mabwawa 50 makubwa na mengine zaidi ya elfu moja ambayo serikali yake inapanga kujenga yanakusudiwa kuvuna na kuhifadhi maji na kubadilisha Kaskazini mwa Kenya kutoka eneo lenye uwezo mdogo kwenda eneo lenye uwezo mkubwa wa maendeleo.

Katika ziara hiyo Rais vile vile alisema Kenya inajenga nyumba za bei nafuu 230,000 kote nchini ili kuwapa wananchi fursa ya kupata makazi bora huku ikikuza ajira na ukuaji jumuishi wa mijini.

Rais alisema mpango huo pia unaimarisha uchumi wa maeneo kwa kutenga sehemu ya kazi—ikiwemo utengenezaji wa milango na madirisha ya chuma—kwa mafundi wa Jua Kali ili faida za kiuchumi zibaki ndani ya jamii.

Kiongozi wa nchi jana alizindua ujenzi wa nyumba za gharama nafuu huko Masalani, mradi ulio na nyumba 376.

Share This Article