Waziri wa Jinsia, Utamaduni na Huduma za Watoto Hanna Wendot Cheptumo, amesema kuwa atatumia nafasi ya kazi yake kutafuta raslimali kutoka kwa serikali na washirika wengine kwa lengo la kuboresha utendakazi wa wizara yake.
Aliyasema hayo alipozindua rasmi mpango wa miaka mitano wa “Usawa Awards” wa Tume ya Kitaifa ya Jinsia na Usawa (NGEC) jijini Nairobi.
Akihutubia mkutano huo, Hanna alisema kuwa wizara hiyo na NGEC hupokea mgao mdogo wa bajeti ya kitaifa ikilinganishwa na majukumu waliyotwikwa.
“Ila kufanya vyema, Mabibi na Mabwana, lazima tuunge maazimio haya kwa rasilimali. Nataka niwahakikishie kwamba nitatumia sauti yangu katika meza ya wizara kuinua nguzo za jinsia, majukumu husika na kutafuta rasilimali za matumizi. Ni wazi kuwa taasisi hizi hupokea mgao mdogo ikilinganishwa na taasisi zingine za serikali licha kuwa majukumu yazo yanahusu walio kwenye mazingira magumu na ambao wanastahili kupata raslimali zaidi,” alisema Hanna.
Pia alifichua kuwa serikali imefungua afisi katika kaunti 46 zitakazotoa huduma kwa walengwa kwa ushirikiano na NGEC na washirika wengine huku akisifia juhudi tele zinazotekelezwa na NGEC katika kupigania haki na kutambua dhuluma na manyanyaso yanayowasonga walemavu, watoto, vijana, wanawake na hata wanaume katika familia, ndoa na sehemu za kazi.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa NGEC Rehema Dida Jaldesa, alisema kuwa, kando na mpango huo kuwatuza watu binafsi, mashirika, taasisi na makundi mbalimbali ambayo yanatetea haki za waathiriwa, mpango huo ambao utagharimu shilingi bilioni saba, unalenga kukamilisha maazimio ya miaka mitano iliyopita ambayo hayakukamilika kwa sababu ya uhaba wa fedha.
Kwenye mkutano huo, makundi mbalimbali yalituzwa kwa mchango wao wa vita dhidi ya mateso na ukiukaji wa haki za binadamu.
Wengine waliohudhuria ni msemaji wa serikali Isaac Mwaura, mashirika ya kijamii na yale ya kibinafsi, wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa, washirika wa kimaendeleo, mabalozi na wageni wengine waalikwa.