Serikali kununua magunia 321,000 ya ngano kutoka kwa wakulima

Tom Mathinji
1 Min Read
Serikali kununua magunia 321,000 kutoka kwa wakulima.

Serikali imetangaza mipango ya kununua ngano kutoka kwa wakulima, kupitia Halmashauri ya Nafaka na Mazao nchini NCPB.

Katika mkutano ulioandaliwa Jumatatu na wadau, waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe, alisema serikali itanunua magunia  321,000ya ngano kutoka kwa wakulima ambao walikuwa na wasiwasi kuhusu zao hilo.

Kagwe amewaagiza wakulima kuwasilisha zao hilo kwa halmashauri ya NCPB, kuanzia Machi 4, 2025.

Kulingana na waziri huyo, wakulima watakaowasilisha zao hilo, watapokea malipo yao baada ya  muda wa siku 30.

Taarifa kutoka kwa wizara hiyo, iliashiria kuwa NCPB itatia saini mkataba wa maelewano na kampuni za usagaji ngano, kuhakikisha ngano hiyo inakusanywa na malipo kutolewa ndani ya siku 14 hadi 21.

Hata hivyo waziri huyo aliwaonya wale ambao watawasilisha kwa NCPB ngano iliyoagizwa kutoka nje, kwamba watakamatwa kwa kuhujumu mchakato huo.

Waziri huyo alidokeza kuwa serikali inalenga kupunguza uagizaji wa ngano kutoka nje ya nchi, kwa kuhakikisha uzalishaji wa zao hilo unaongezeka kutoka asilimia 8 hadi 40 kutimiza mahitaji ya kampuni za usagaji ngano.

Halmashauri ya NCPB  ina mipango ya uzinduzi wa  hifadhidata, itakayotumiwa kusambaza mbolea ya gharama nafuu kwa wakulima wa ngano, kwa lengo la kupunguza gharama ya uzalishaji.

 

Share This Article