Serikali kukabiliana na tatizo la uvujaji damu kwa wingi baada ya kujifungua

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa.

Waziri wa afya Debora Barasa ametoa wito wa kutekelezwa juhudi za kukabiliana na tatizo la kuvuja damu kwa wingi baada ya kujifungua miongoni mwa kina mama,  maarufu Postpartum Hemorrhage (PPH).

Kulingana na waziri huyo, ipo haja ya kutambua ugonjwa huo mapema na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wakati.

Tatizo hilo limetajwa kuwa chanzo kikuu cha vifo miongoni mwa kina mama wanapojifungua.

Akizungumza Nairobi wakati wa hafla ya uzinduzi wa mbio za mpango wa kukabiliana na tatizo hilo  End PPH Run, Barasa alidokeza kuwa hali hiyo inazidi kusababisha maafa, licha ya juhudi zilizowekwa za kuimarisha huduma za afya za kina mama wajawazito kote nchini.

“Ni lazima tuzuie maafa yanayosababishwa na PPH. Ugundunzi wa mapema utasaidia kuokoa maisha.” alisema Barasa.

Alisema PPH huchangia asilimia 25 hadi 45 ya vifo miongoni mwa kina mama wajawazito hapa nchini.

Waziri Barasa aliangazia hatua kama vile kuimarishwa kwa mpango wa Linda Mama chini ya halmashauri ya afya ya jamii SHA, kama mojawapo wa hatua ambazo zitaimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kina mama wajawazito.

Mbio hizo zimedhamiriwa kutoa amasisho na kutafuta ufadhili kukabiliana na vifo kwa wamama wajawazito kutokana na tatizo la PPH.

Share This Article