Msemaji wa serikali Isaac Mwaura amezungumzia mipango kadhaa ya serikali inayolenga kuhakikisha usalama wa Wakenya na uthabiti endelevu wa uchumi wa taifa.
Katika taarifa yake ya leo, Mwaura alizungumzia hatua ya hivi maajuzi ya Marekani kujiondoa kwenye Shirika la Afya Duniani (WHO) na hivyo kukatiza ufadhili wa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi.
Alihakikishia waathiriwa wa hatua hiyo kwamba serikali inakusanya mapato ya kununua dawa hizo huku ikitafuta washirika wapya ndiposa upatikanaji wa dawa hizo uendelee bila tatizo.
“Afya yenu na usalama wenu ni vipaumbele kwetu,” alisisitiza msemaji huyo wa serikali.
Kuhusu ongezeko la mauaji ya wanawake nchini, serikali imezindua jopo kazi la kukomesha visa hivyo vya dhuluma za kijinsia kuhakikisha umakini na hatua spesheli katika kusimamia uovu huo katika jamii.
Katika kupiga jeki ukuaji wa uchumi, Mwaura alizungumzia mafanikio ya mpango wa Inua Jamii wa kugawa pesa kwa wasiojiweza katika jamii akisema shilingi bilioni 3.52 ziligawiwa watu milioni 1.7, Disemba 2024.
Kulingana naye, hatua ya kuanza kutumia MPESA kugawa pesa hizo inalenga kuimarisha ufanisi na upatikanaji wa fedha hizo.
Serikali imethibitisha pia kujitolea kwake kwa kilimo ikiangazia uwekezaji katika viwango mbalimbali vya uzalishaji, ruzuku ya pembejeo na juhudi za kupunguza bei ya vyakula.
Mwaura alisema kwamba sasa Kenya imejitosheleza kwa mahindi na mfumko wa bei za vyakula ni wa kiwango cha chini kabisa katika muda wa miaka mitatu iliyopita.
Sekta ya mifugo pia iliangaziwa na msemaji wa serikali ambaye alizungumzia usimamizi wa mkurupuko wa ugonjwa wa miguu na midomo katika kaunti kadhaa nchini.
Alisema serikali imeanzisha hatua kadhaa za kudhibiti hali hiyo huku mpango wa nchi nzima wa utoaji chanjo ukitarajiwa ili kulinda mifugo na kuhakikisha bidhaa za mifugo za humu nchini zinakubalika katika masoko ya kimataifa.
Mpango huo utalenga mamilioni ya mifugo kuimarisha afya yao na kulinda riziki ya wafugaji.
Mwaura alisema kwamba mfumko wa bei za bidhaa umeshuka hadi asilimia 2.7 huku viwango vya riba pia vikipungua na hivyo kuhimiza uwekezaji.
Serikali inahimiza wananchi kuunga mkono mipango yake kwa ajili ya mazuri kwa taifa zima.