Serikali inalenga kuandikisha wanafunzi wapya wapatao milioni mbili katika taasisi za Mafunzo ya Ufundi na Ufundistadi (TVET) kufikia mwisho wa mwaka ujao, ikiwa ni juhudi za kuwapa vijana wanaohitimu kutoka shule za sekondari ujuzi wa kiufundi na kuwawezesha kuanzisha ajira zao wenyewe.
Waziri wa Elimu, Julius Ogamba alitoa tangazo hilo wakati wa mahafali ya pili katika Chuo cha Kitaifa cha Ufundi cha Nyandarua ambapo zaidi ya wahitimu 1,500 walituzwa vyeti na diploma katika fani mbalimbali za kiufundi.
“Tunataka vijana wengi zaidi wajifunze ujuzi wa kiufundi. Ndiyo maana tumeweka lengo la kuwaandikisha wanafunzi milioni mbili. Serikali imetenga fedha za kutosha kufanikisha mpango huu,” alisema Waziri Ogamba.
Aliwahimiza wahitimu kutumia maarifa waliyojifunza kuunda nafasi mpya za ajira badala ya kutegemea kuajiriwa.
“Haupaswi kutoka hapa na kutegemea kupata ajira mara moja. Tumia ubunifu wako na ujuzi uliopata hapa kuanzisha biashara na ajira mpya. Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa biashara ili kuwawezesha,” aliongeza.

Kwa lengo la kuboresha elimu ya sayansi na teknolojia (STEM), Ogamba alitangaza kuwa shule zote za sekondari ambazo bado hazina maabara zitapatiwa vifaa ifikapo mwisho wa mwaka ujao.
“Tumeweka fedha za kutosha kwa mradi huu. Tunataka kuhakikisha kuwa vijana wetu wanapata ujuzi wa vitendo kabla ya kuhitimu sekondari, ili kuwapa mwelekeo sahihi wa kitaaluma.”
Aidha, Waziri Ogamba alisema kuwa wizara yake imeanzisha zoezi la uhakiki katika sekta zote za elimu ili kudhibiti matumizi ya takwimu potovu, hasa katika ajira ya walimu na maendeleo ya miundombinu.
Waziri wa Utalii Rebecca Miano,ambaye aliandamana naye, aliwahimiza wahitimu kutafuta fursa za ajira na uwekezaji katika sekta ya utalii ambayo bado haijatumika ipasavyo.
“Sektaya utalii ni injini ya ukuaji wa uchumi – hata katika wizara ninayoiongoza. Maeneo kama vile Ziwa Olbolosat na arboretamu ya Nyandarua – ambayo ni ya kipekee nje ya Nairobi – yanatoa fursa zisizo na kikomo. Serikali ipo tayari kusaidia vijana kuingia katika sekta hii,” alisema Miano.
Aliwahimiza wahitimu kutumia nafasi yao ya kipekee kushiriki katika ukuaji wa uchumi wa taifa kwa njia ya ubunifu na ujasiriamali.

Hata hivyo, changamoto kama vile ukosefu wa maji, uhaba wa hosteli, na miundombinu duni kama ukosefu wa madaraja ya watembea kwa miguu bado zinakabili Chuo cha Kitaifa cha Ufundi cha Nyandarua.
Dkt. Felix Mung’atu, Mkuu wa Chuo hicho alieleza mafanikio yaliyopatikana ikiwemo ushirikiano wa kimataifa na utafiti unaolenga kuboresha jamii.
“Tumewezesha wanafunzi wetu wengi kupata nafasi ya kwenda Uingereza, Mashariki ya Kati, na Kuwait. Tunajihusisha kikamilifu na utafiti. Tayari tumetengeneza unga ulioimarishwa kwa lishe bora na dawa ya kuua wadudu wa kilimo kwa njia ya asili. Sasa tunatafuta washirika kusaidia kuviendeleza na kuvibadilisha kuwa bidhaa za kibiashara,” alisema Dkt. Mung’atu.
Miongoni mwa wahitimu waliohudhuria, ni Caleb Bogonko kutoka Idara ya Kilimo cha Jumla, ambaye alishiriki hadithi yake ya mafanikio.
“Kupitia mpango unaodhaminiwa na chuo, nimepata nafasi ya kusafiri hadi Uingereza mara mbili. Mpango huu huturuhusu kusoma kwa miezi sita darasani na kisha miezi sita mingine kupata mafunzo ya vitendo Uingereza. Maarifa niliyopata hapa Nyandarua National Polytechnic yamenisaidia kung’aa kimataifa,” alisema Bogonko.
Aliongeza kuwa zaidi ya wahitimu 200 kutoka chuo hicho kwa sasa wanafanya kazi Uingereza na Mashariki ya Kati, jambo linalodhihirisha ubora wa mafunzo yanayotolewa katika taasisi hiyo ya TVET.