Serikali itazisaidia familia za waathiriwa wa maporomoko ya ardhi Marakwet

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen akiwahutubia wakazi wa kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Serikali imesema itazisaidia familia za waathiriwa wa maporomoko ya ardhi yaliyotokea katika eneo la Chesongoch, Marakkwet Mashariki, kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen alidokeza kuwa serikali itaharakisha ukarabati wa miundo mbinu na usaidizi wa kibinadamu kuhakikisha familia zilizoathirika zinarejelea maisha yao ya kawaida haraka iwezekananvyo.

Murkomen aliyasema hayo Jumamosi alipotembelea familia zilizoathirika na mkasa huo katika eneo la Embobut.

“Licha ya kupotea kwa maisha, makazi yaliharibiwa, mashamba, mifugo na mimea ilisombwa na maji,” alisema waziri huyo.

Kulingana na waziri huyo, barabara kuu inayoelekea katika eneo hilo iliharibiwa na maji na vifursi.

Aidha, waziri huyo alitoa wito wa kubainishwa kwa maeneo ya kiikolojia ili kukuza mimea itakayosaidia kurejesha mifumo ikolojia iliyoharibiwa.

Alisema kuwa mimea kama vile kahawa, majani chai na miti ya matunda inaweza kusaidia kurejesha mifumo ikolojia akiongeza kusema kuwa mimea mingine ya nafaka inaweza kukuzwa kwenye mabonde.

Kwenye ziara hiyo, Murkomen alikuwa ameandamana na Gavana Wisley Rotich, wabunge Caroline Ng’elechei na Adams Kipsanai miongoni mwa viongozi wengine na maafisa wa serikali.

Share This Article