Serikali itashinikiza Marekani kuongeza muda wa AGOA

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa biashara Lee Kinyanjui.

Waziri wa Biashara, Uwekezaji na Viwanda Lee Kinyanjui, amewahakikishia wadau katika sekta ya nguo kwamba serikali inajizatiti kushinikiza kuongezwa kwa muda wa kibiashara wa AGOA na Marekani.

Akiwahutubia wadau wa sekta ya nguo hapa nchini katika hoteli moja Nairobi, Kinyanjui alisema hatua ya hivi karibuni ya kuongezwa kwa asilimia 10 kwa bidhaa za Kenya zinazoingia Marekani, kumesababisha changamoto kubwa katika sekta hiyo, na ipo haja ya swala hilo kushughulikiwa kwa dharura.

Waziri huyo alidokeza kuwa awali bidhaa za Kenya hazikutozwa ushuru chini ya mpango wa AGOA, lakini sasa hali ni tofauti na huenda ikaathiri ushindani wa bei kwa bidhaa za hapa nchini na kuhujumu mikataba ya biashara.

Mpango wa sasa ambao unaruhusu bidhaa za Kenya kuingia Marekani bila kutozwa ushuru, unakamilika mwezi Septemba mwaka huu.

Kinyanjui alisema serikali kwa ushirikiano na Chama cha Watengenezaji Bidhaa nchini (KAM), zinashinikiza kuongezwa kwa muda huo ili kuimarisha manufaa ya kiuchumi.

Share This Article