Rais William Ruto ametangaza kuwa, serikali itazindua hazina ya miundombinu hivi karibuni, itakayotumiwa kufadhili miradi mikubwa ya miundombinu inayotekelezwa na taifa hili.
Akihutubia taifa wakati wa maadhimisho ya 62 ya Siku Kuu ya Mashujaa katika kaunti ya Kitui, kiongozi wa taifa alieleza kuwa hazina hiyo itaiwezesha serikali kufadhili miradi kama vile ujenzi wa mabwawa, barabara, reli na viwanja vya michezo.
“Tuna rasilimali zinazoweza kupeleka taifa hili mbele. Tutawasilisha hoja bungeni kubuniwa kwa hazina ya miundombinu itakayofadhiliwa na ushuru wetu, fedha za ubinafsishaji na kutoka kwa washira wa kimaendeleo,” alisema Rais Ruto.
Ruto pia alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi rasilimali kwa ajili ya mahitaji ya siku zijazo.
Alisema maeneo matatu ambayo yamepewa kipaumbele kwa maendeleo endelevu ya taifa hili ni kuimarisha akiba ya chakula, kukuza uchakataji wa mazao na uendelezaji wa viwanda, na kupanua uwezo wa nishati endelevu pamoja na maendeleo ya miundombinu ili kuharakisha ukuaji wa uchumi.