Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi amesema serikali inajizatiti kukabiliana na zimwi la misongamano jijini Nairobi.
Mudavadi aliyepia waziri wa Mambo ya Nje, aliangazia kwa kina hatua muhimu ambazo zinatarajiwa kuchukuliwa ili kuboresha mfumo wa uchukuzi Nairobi.
Aliyasema hayo alipokutana na washirika wa kimataifa wa maendeleo, akiwa ameandamana na Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir katika jumba la Railways, Nairobi.
“Majadiliano yetu na mabalozi wa nchi za nje pamoja na washirika wetu wa kimaendeleo wakiongozwa na Balozi wa Uingereza hapa nchini Neil Wigan, yaliangazia kwa kina lengo la kuimarisha miundombinu ya Nairobi kupitia ushirikiano, uvumbuzi na uwajibikaji,” alisema Mudavadi.
Mudavadi alitoa wito kwa wadau kuimarisha ushirikiano huku taifa hili linapopiga hatua za kimaendeleo na kuimarisha miundombinu ya jiji la Nairobi.
“Tumesalia imara kuboresha mpango huo, ukiwa nguzo muhimu katika hatua za maendeleo ya Kenya,” alidokeza Waziri huyo.