Serikali imesema imefunga kampuni bandia 600 zinazotoa ajira ughaibuni, ili kuwalinda wakenya wanaofanya kazi nje ya nchi hii.
Akizungumza alipokutana na wakenya wanaoishi nchini Qatar, Rais William Ruto alisema sasa wakenya wanatafutiwa ajira kwa nchi ambazo zina mkataba rasmi za ajira na Kenya.
“Tunaendelea kutafuta mikataba mipya ili kutoa fursa za ajira kwa wakenya nje ya nchi, kuwawezesha vijana wetu kupata kazi zilizo na malipo ya kumezewa mate, wapate ujuzi watakaouleta nyumbani,” alisema kiongozi wa nchi.
Rais alisema serikali inajizatiti kuwawezesha wakenya wanaofanya kazi nje ya nchi kuchangia katika ukuaji wa taifa hili, huku ikitekeleza mbinu za kuwawezesha kutuma fedha nchini Kenya kwa gharama nafuu ili kupanua mifumo ya uwekezaji.
“Tumepunguza muda wa kutoa pasipoti kutoka miezi tatu hadi siku tatu kwa wale ambao wamepata ajira nje ya nchi, na tunafanikisha usafiri wao,” aliongeza Rais Ruto.
Rais Ruto yuko nchini Qatar kuhudhuria mkutano waUmoja wa Mataifa kuhusu ustawi wa Jamii, ambapo pia anapigia debe uwekezaji wa kigeni hapa nchini.