Serikali haitarejeshe ule mfumo wa kuwachunguza wakenya wanaoishi sehemu za mpakani wakati wa utoaji vitambulisho vya taifa, hayo ni kwa mujibu wa NaibuRais Prof. Kithure Kindiki.
Naibu huyo wa Rais alisema hatua ya Rais William Ruto itaendelea kutekelezwa, na ilinuia kuondoa ubaguzi uliolenga baadhi ya jamii za hapa nchini.
Aliyasema hayo Jumanne, alipokuwa mwenyeji wa Wabunge kutoka Kaskazini mwa Kenya katika makazi yake rasmi ya Karen, ili kujadili miradi ya maendeleo inayoedelea katika eneo hilo.
“Nimeridhishwa na sera iliyoondolea mbali ubaguzi katika utoaji wa Vitambulisho vya Taifa,” alisema Prof. Kindiki.
Wakati huo huo, Kindiki alisema serikali inatekeleza ajenda ya maendeleo isiyo na ubaguzi, akidokeza kuwa yeye anapigia debe usawa wa Wakenya wote.
“Ninaamini kila sehemu ya Kenya inapaswa kuhudumiwa kwa usawa, na sehemu zilizosalia nyuma zinapaswa kushughulikiwa na serikali,” alisema Kindiki.