Senge Hellena kutangaza eneo jipya la onyesho lake jijini Eldoret

Usimamizi wa eneo alilokuwa ametangaza wali ulibatilisha makubaliano yao kwa sababu za kiusalama.

Marion Bosire
2 Min Read
Senge Hellena

Waandalizi wa onyesho la vichekesho lililopatiwa jina la “Tos Majehovah” la mwigizaji na mchekeshaji wa mitandaoni Senge Hellena wanatizamiwa kutangaza eneo jipya la kuliandaa.

Awali onyesho hilo la Agosti 2, 2025 lilikuwa limepangiwa kuandaliwa katika eneo la Eldoret Sports Club, lakini usimamizi wa eneo hilo ukalitupilia mbali.

Tangazo la usimamizi wa Eldoret Sports Club la Juni 27, 2025, lililotiwa saini na katibu Samson Changwony lilitaja usalama kuwa sababu kuu ya kufutilia mbali uandaaji wa onyesho hilo.

Senge Hellena na kundi lake pia walitoa taarifa rasmi na kusema kwamba onyesho hilo litafanyika kama ilivyopangwa katika eneo litakalotangazwa baadaye jijini Eldoret.

Msanii huyo ambaye ni wa kiume kwa jina halisi Vitalis Kiplagat lakini anaigiza kama shangazi, anahakikishia mashabiki na washirika wake kwamba eneo jipya litatangazwa hivi karibuni.

“Tumejitolea kuwaandalia onyesho salama, la kuburudisha na la athari nzuri” walisema waandalizi wa onyesho hilo katika taarifa rasmi.

Walishukuru usimamizi wa Eldoret Sports Club kwa ushirikiano wa awali na kuonyesha utayari wa kushirikiana tena katika siku za usoni.

Awali, Senge Hellena alijipata pabaya kwa kushiriki maandamano ya Julai 25, 2025 yaliyoandaliwa kama njia ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024.

Yalikuwa pia ya kukumbuka waliofariki kwenye maandamano hayo ambapo waandamanaji walivunja sehemu ya ua unaozunguka bunge na kuingia humo.

Kampeni ilianzishwa mitandaoni ya kuhimiza mashabiki kumsusia Senge huku watumizi wengine wa mitandao na wasanii wenza wakimtetea na kuhimiza watu kumfuatilia.

Share This Article