Bunge la Seneti lilimwokoa Gavana wa kaunti ya Kericho Eric Mutai kutokana na jaribio la kumbandua madarakani kwa mara ya pili jana usiku.
Sababu kuu ya maseneta kupinga pendekezo la kung’atuliwa madarakani kwa Gavana Mutai ni suala la ukosefu wa idadi inayohitajika ya thuluthi mbili za wawakilishi bunge wakati wa upigaji kura ya kumbandua madarakani.
Baada ya siku tatu za maamuzi, maseneta walikabiliwa na suala la upigaji kura na idadi ya wabunge waliokuwa katika bunge la kaunti ya Kericho wakati wa kupitisha hija hiyo.
Wawakilishi wadi wa Kericho walikuwa wameorodhesha makosa matatu dhidi ya Gavana Mutai ambayo ni ukiukaji wa katiba na sheria nyingine, matumizi mabaya ya mamlaka na uptovu wa maadili.
Gavana aliwasilisha mashahidi wapatao 20 katika kujitetea 18 kati yao wakiwa wawakilishi wadi waliokanusha kupiga kura siku hiyo wakisema mfumo wa kupiga kura kielektroniki ulivurugwa na wakapigiwa kura bila idhini yao.
Upande wa bunge la kaunti ta Kericho ulikuwa na mashahidi sita huku Seneti ikiamua kutafuta huduma za mjuzi huru wa teknolojia kutoka kwa mamlaka ya teknolojia ya mawasiliano nchini.
Maseneta 26 walipinga kuondolewa afisini kwa Gavana Mutai kutokana na hali ya upigaji kura kutoweza kuthibitika na hivyo kuifanya iwe vigumu kufahamu iwapo shughuli hiyo ilitekelezwa.
Bunge ka Seneti lilimwokoa tena Gavana Mutai kutokana na hoja ya kumwondoa afisini Oktoba mwaka uliopita wa 2024.