Seneta mteule Consolata Nabwire Wakwabubi ameapishwa rasmi leo katika kikao maalum cha bunge la Seneti baada ya kuteuliwa na chama cha UDA.
Wakwabubi mkazi wa kaunti ya Bungoma ameteuliwa chini ya kifungu nambari 98 sehemu ya kwanza (b) cha katiba ya Kenya kuwakilisha wanawake katika bunge la Seneti ambapo anachukua mahala pa Gloria Orwoba.
Orwoba aliondolewa kwenye sajili ya wanachama wa chama hicho cha UDA na hivyo kusababisha apoteze wadhifa wake wa Seneta mteule.
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC ilirasimisha uteuzi wa Wakwabubi kupitia chapisho kwenye gazeti rasmi la serikali Ijumaa Agosti 15, 2025 na hivyo kutoa fursa kwa uapisho wake.
Walipokuwa wakimkaribisha maseneta walimhimiza azingatie kanuni za bunge la Seneti akikumbuka fika kilichosababisha mtangulizi wake apoteze wadhifa wake.
Seneta wa kaunti ya Nairobi Edwin Sifuna alimkaribisha Wakwabubi Nairobi akisema kwamba yuko salama bora tu ajue kutaja jina “Sifuna” kauli iliyochekesha maseneta.
Enoch Wambua anayewakilisha kaunti ya Kitui katika Seneti alimrejelea Seneta Nabwire kama binamu alipokuwa akimkaribisha huku akitania Seneta wa Nyamira Okong’o Mogeni kwamba hana furaha kwani wamepoteza fursa bungeni kufuatia kuondolewa kwa Orwoba.
Orwoba alikuwa ameashiria kwamba ataelekea mahakamani kupinga uamuzi wa kumwondoa kwenye wadhifa wake.