Mwanamuziki wa mtindo wa rap nchini Marekani Sean Kingston alihukumiwa kifungo cha miaka 3 unusu jela Ijumaa kuhusiana na ulaghai wa dola milioni 1, ambapo alitumia umaarufu wake kupata bidhaa za kifahari.
Bidhaa hizo zinajumuisha gari aina ya Cadillac Escalade lisilopenya risasi huku akikosa kulipa wauzaji.
Serikali ya Marekani ilisema kwamba Kingston wa umri wa miaka 35 ambaye jina lake halisi ni Kisean Anderson, alihadaa wahanga kwa kuwashawishi kumpatia televisheni ya inchi 232 aina ya LED, saa za kifahari na bidhaa nyingine za thamani kwa ahadi ya kuwalipa, lakini alituma miamala ya uongo ya benki.
Mamake aitwaye Janice Turner, alihusika kwenye ulaghai huo, kulingana na wachunguzi, ambao walisema wawili hao walitumia umaarufu wa Kingston na ushawishi wake katika mitandao ya kijamii kuwafanya wahanga wao wasichunguze kwa kina.
Mnamo Machi, baraza la mahakama la Florida Kusini liliwapata na hatia wote wawili kwa makosa matano ya jinai, yakiwemo udanganyifu kwa njia ya mtandao na njama ya kutekeleza udanganyifu huo.
Mwezi Julai, Turner wa umri wa miaka 62, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela na anaendelea kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Wakati wa hukumu katika Mahakama ya Wilaya ya Marekani mjini Fort Lauderdale, Kingston, ambaye alipata umaarufu kupitia kibao chake cha mwaka 2007, “Beautiful Girls,” aliomba msamaha kwa ulaghai huo, ambao wakili wake alisema katika hati ya hukumu kuwa haukuwa wa vurugu na hivyo ulipaswa kupatiwa adhabu nyepesi.
Wakili huyo, Zeljka Bozanic, alipendekeza Kingston apewe kifungo cha nyumbani na akamwelezea mteja wake kuwa “mwenye majuto makubwa.”
Lakini baada ya kikao cha dakika 70 mbele ya Jaji David S. Leibowitz siku ya Ijumaa, Kingston alijulishwa kwamba atakwenda jela.
“Sean anachukulia hili kama somo na ataendelea mbele kwa njia chanya,” Bozanic aliandika katika barua pepe siku ya Ijumaa.
Bozanic alisema kuwa sehemu kubwa ya fedha za fidia katika mpango huo tayari zilikuwa zimerudishwa na Kingston, ambaye alikuwa anakabiliwa na hukumu ya hadi miaka 20 kwa kila kosa kati ya makosa matano.
Alisema kuwa Kingston bado anatafakari fursa alizo nazo kisheria, ikiwa ni pamoja na kukata rufaa.
Afisi ya Mwanasheria wa Serikali ya Marekani kwa Kanda ya Kusini mwa Florida haikujibu mara moja maombi ya maoni siku ya Ijumaa kuhusu hukumu ya Kingston.
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, Marc Anton, naibu mwanasheria wa serikali ya Marekani, alisema kuwa Kingston alikuwa amezoea maisha ya umaarufu lakini alikuwa akiishi zaidi ya uwezo wake, shirika la habari la Associated Press liliripoti.
“Ni wazi kwamba hapendi kulipa na hutegemea umaarufu wake kuwadanganya wahanga wake,” Anton alisema. “Yeye ni mwizi na tapeli, kwa maneno rahisi.”
Mnamo Mei 2024, kikosi maalum cha SWAT kilivamia nyumba ya Kingston katika Kaunti ya Broward, Florida, na kumtia mama yake mbaroni.
Rapa huyo alikuwa akitumbuiza Kusini mwa California katika kambi ya mafunzo ya jeshi ya Fort Irwin, katika Jangwa la Mojave, wakati alipokamatwa.
Katika kesi ya madai iliyowasilishwa miezi michache kabla, kampuni inayouza na kufunga mifumo ya burudani ya hali ya juu ilimshutumu Kingston kwa ulaghai na kuvunja mkataba kwa kushindwa kulipa kwa televisheni ya inchi 232 na “mfumo wa sauti wa hali ya juu” uliowekwa nyumbani kwake Septemba 2023.
Kampuni hiyo, Ver Ver Entertainment, ilisema katika kesi hiyo kuwa, kama sehemu ya makubaliano ya kupunguza malipo ya awali, Kingston aliahidi kutumia mahusiano yake ya kimuziki kumshawishi Justin Bieber kutengeneza video za matangazo kwa ajili ya biashara hiyo.
Video hizo hazikutokea, kulingana na kesi hiyo, ambayo ilisema kuwa Kingston alikuwa amelipa tu dola 30,000 kati ya dola 115,000 alizodaiwa kwa mfumo huo. Kesi hiyo bado inaendelea.
Kingston, alipokuwa kijana, alipanda hadi nafasi ya kwanza kwenye chati ya Billboard Hot 100 mwaka 2007 kupitia wimbo wake wa kwanza, “Beautiful Girls,” ambao ulitumia sampuli kutoka wimbo wa Ben E. King “Stand By Me.”
Kingston, ambaye alizaliwa Florida na kukulia Jamaica, amewahi kushirikiana na wasanii mashuhuri kama Justin Bieber, Nicki Minaj na Wyclef Jean.