Mwigizaji Sandra dacha amejibu wakosoaji ambao wamemsema sana mitandaoni wakidai kwamba yeye hupatikana kwa urahisi kusaidia watu na kuhudhuria hafla hatua ambayo huenda ikashusha thamani yake.
Haya yanajiri baada ya wakosoaji wa mitandaoni akiwemo Nyako kuchambua hafla ya Jumapili ya ndoa ya kitamaduni ya mwanamuziki Prince Indah na mkewe Winnie katika eneo la Rapogi kaunti ya Migori.
Akizungumza mubashara kwenye mtandao wa TikTok, Nyako alidai kwamba hafla hiyo ya Indah hata ingawa inasifiwa na wengi haikuafikia viwango ambavyo alitarajia.
Baadaye alimchambua Dacha akisema yeye hupatikana katika kila hafla na mara nyingi huwa mstari wa mbele iwe harusi, matanga au hata mchango.
Wapo wanamitandao waliokubaliana na Nyako huku wengine wakimtetea Dacha kwa kuwa rafiki mzuri.
Kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, Dacha alijibu ukosoaji huo kwa hoja tano. Alianza kwa kusema kwamba yeye ni rafiki ambaye yupo kila mara anapohitajika.
“Sio makosa yangu kwamba marafiki wenu hawafanyi harusi kila mara.” ndilo jibu la pili alilotoa Dacha huku akicheka huku akiongeza kwamba wakosoaji wanastahili kushukuru kwamba hakuna marafiki wao ambao wanakufa au kufiwa na wapendwa wao.
Mwigizaji huyo wa muda mrefu alisema pia kwamba ataendelea kuhudhuria hafla zote za marafiki iwe harusi iwe matanga na kwamba hakuna lolote ambalo wakosoaji wanaweza kufanya.
Alimalizia kufafanua kwamba yeye huwa pia anajihusisha na fani ya maandalizi ya hafla mbali mbali na akatoa nambari yake ya simu ili yeyote ambaye anahitaji huduma zake aweze kuwasiliana naye.