Sammy Mwaita afikishwa kortini kwa ulaghai wa ardhi ya shilingi milioni 150

Martin Mwanje
2 Min Read
Mbunge wa zamani wa Baringo Central Sammy Mwaita akiwa mahakamani

Mbunge wa zamani wa Baringo Central Sammy Mwaita leo Jumatatu amefikishwa katika mahakama ya Milimani akikabiliwa na mashtaka mbalimbali yanayohusu unyakuzi wa ardhi yenye thamani ya shilingi milioni 150. 

Mwaita, ambaye wakati mmoja alihudumu kama Kamishna wa Ardhi, alikamatwa katika eneo la Kilimani jijini Nairobi jana Jumapili na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI.

Mwaita alishtakiwa kwa kutengeneza hatimiliki mbili za ardhi kinyume cha sheria kwa lengo la kuwalaghai wamiliki halisi wa vipande hivyo viwili vya ardhi.

Upande wa mashtaka uliiambia mahakama kwamba Mwaita na mshtakiwa mwenza, Brian Kiptoo Kiplangat, walikula njama Machi 30, 2001 au kabla ya tarehe hiyo kutengeneza nyaraka kwa ajili ya Hatimiliki Kuu yenye nambari ya usajili  209/9968 IR No. 85847 bila mamlaka ya kisheria.

Nyaraka hizo za kughushi zilinuiwa kumlaghai Rose Njoki King’au anayemiliki ardhi ambayo imeainishwa kama kipande cha ardhi Namba “A”.

Upande wa mashtaka pia ulifichua kuwa Mwaita, wakati akihumu katika ofisi ya umma, alisajili kinyume cha sheria kipande hicho cha ardhi pamoja na kipande kilichopo karibu kilichotambuliwa kama “B”, bila idhini au ufahamu wa wamiliki wake Rose Njoki King’au na Micugu Wagatharia.

Kitendo hicho kimetajwa na upande wa mashtaka kuwa matumizi mabaya ya mamlaka.

Mbali na mashtaka ya ulaghai, Mwaita pia anakabiliwa na mashtaka mengine kadhaa ikiwa ni pamoja na kupanga kutekeleza uhalifu, kubuni stakabadhi bila idhini, utumizi mbaya wa mamlaka na kutoa habari za kupotosha kwa afisa wa umma.

Kiplagat ambaye ni mshtakiwa mwenza wa Mwaita hakufika mahakamani kukiri mashtaka na kumchochea Hakimu Mkuu Mwandamizi anayesikiliza kesi dhidi yao Ben Mark Ekhubi kumtaka kufika mahakamani kesho Jumanne.

Mwaita alikanusha mashtaka dhidi yake na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 10 au dhamana mbadala ya pesa taslimu milioni 2.

 

Share This Article