Samidoh amwomboleza Ngugi Wa Thiong’o

Alikumbuka alivyokutana na kushauriana naye mwaka jana nchini Marekani.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa mtindo wa Mugithi Samuel Muchoki maarufu kama Samidoh amemwomboleza mwandishi na msomi maarufu Ngugi Wa Thiong’o.

Kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, Samidoh alichapisha picha alizopigwa awali na Ngugi huku akielezea huzuni aliyokuwa nayo baada ya kupokea taarifa za kifo chake kilichotokea jana.

“Ni kwa masikitiko makubwa nimepokea habari za kifo cha mtu wa maana na mhifadhi wa utamaduni wetu, Profesa Ngugi wa Thiongo,” aliandika Samidoh.

Afisa huyo wa polisi ambaye anaripotiwa kuadhibiwa kwa kuhamishwa alisema kwamba mwezi Juni mwaka jana alisafiri hadi Atlanta, Georgia kuhudhuria hafla iliyokuwa imepangwa ya kumuenzi Thiong’o.

“Tulikuwa na majadiliano ya maana kuhusu kazi zake hasa zile alizoandika kukashifu utawala mbaya nchini alisema Samidoh katika chapisho lake.

Kulingana naye, Ngugi alitekeleza jukumu muhimu katika kumtia moyo kuendeleza sanaa yake katika lugha yake asilia ya Kikuyu ambapo alimwambia kwamba ana athari nzuri kwa jamii yake.

Alilalamika kwamba alikuwa ameahidi kurejea Marekani kumzuru ili amsaidie kuhariri kitabu chake ambacho anaendelea kuandika lakini hili sasa halitafanyika.

Mwanamuziki huyo alimalizia kusema kwamba kama nchi na jamii kwa jumla tumepoteza mtu wa maana sana.

Ngugi Wa Thiong’o aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87.

Share This Article