Samba Mapangala asema bado yupo

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa Rhumba toka nchini Congo Samba Omar Mapangala amehakikishia mashabiki wake kwamba bado yupo na anaendelea kutoa muziki.

Samba alitumia akaunti yake ya mtandao wa kijamii Facebook kutoa habari hizo ambapo alichapisha picha zake za sasa akisema, “Mashabiki wangu wanauliza kama bado niko hai na kama naendelea na muziki”.

Aliendelea kwa kujibu swali hilo akisema hajawahi kukoma kuendeleza burudani na kwamba yuko hai huku akiwashauri wapate kazi zake mpya kwenye mtandao wa YouTube.

Msanii huyo ambaye sasa anaishi nchini Marekani alijipatia umaarufu na muziki wake katika eneo la Afrika Mashariki miaka ya 1980 akiwa kiongozi wa bendi iliyoitwa Orchestra Virunga, ambayo alianzisha akiwa nchini Kenya.

Mwimbaji huyo wa wimbo maarufu wa Vunja Mifupa alizaliwa katika eneo la Matadi nchini Congo, akalelewa na kusoma jijini Kinshasa.

Baada ya masomo alijiunga na bendi kadhaa za muziki nchini Congo kama Super Tukina, Super Bella Bella, Bariza na Saka Saka kabla ya kuhamia nchini Uganda.

Yeye na wenzake wa asili ya Congo walianzisha bendi iitwayo Les Kinois nchini Uganda ambapo walikaa kwa muda wa miaka miwili hivi kabla ya kuhamia Nairobi nchini Kenya.

Mwaka 1981 ndio alianzisha bendi ya Orchestra Virunga ambayo aliipa jina la Volcano ya Virunga iliyopo nchini Congo.

Alabamu ya kwanza ya bendi hiyo iitwayo “It’s Disco Time” ilitolewa mwaka 1982. Ilipofika miaka ya 1990 bendi hiyo ilijipatia umaarufu kimataifa.

Kufikia miaka ya 2000 bendi hiyo ilianza kupotea pole pole ndiposa mashabiki wakawa wanashangaa iwapo wahusika wapo.

Mapangala ana kazi nyingi mpya ambazo ametoa katika miaka ya hivi maajuzi akiwa Marekani na amezichapisha kwenye akaunti yake ya YouTube.

Share This Article