Mbunge wa Mumias mashariki Peter kalerwa Salasya ametangaza rasmi kwamba atawania rais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Akihutubia wanahabari jijini Nairobi, Salasya alisema kuwa uamuzi wake unafuatia changamoto mbali mbali za maisha zinazowakumba wananchi.
“Wakenya wenzangu, marafiki na wazalendo, leo ninasimama mbele yenu kwa unyenyekevu, ujasiri na mvuto mkuu kutangaza kuwa, mimi muheshimiwa Peter Kalerwa Salasya mjumbe wa Mumias Mashariki natangaza rasmi kuwania kiti cha urais wa jamuhuri ya Kenya katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2027” Alisema Salasya.
Mbunge huyo aliendelea kusema kwamba wakati huu si kuhusu yeye bali ni wananchi; wakenya wa kawaida, wafanyikazi wa umma ambao mishahara yao inapungua kwa sababu ya ushuru wa adhabu, wakulima wanaosumbuka kupata mbolea, mama anayechagua kati ya chakula na dawa,mahafala wanaotuma wasifu bila kujibiwa na vijana wa Gen Z wanaotaka serikali ya usawa.
Mbunge huyo wa awamu ya kwanza alifichua kuwa iwapo atanyakua wadhifa huo, atapunguza ushuru, kupanua nafasi za ajira na ushirikiano wa vijana na serikali, kuboresha mfumo wa matibabu, elimu, taasisi za serikali na kumaliza ufisadi.
Tangazo hilo, limepokelewa kwa kauli mseto na wakenya wa tabaka mbali mbali. Baadhi wamempongeza kwa ushujaa huo huku wengine wakimshauri asalie kwenye wadhifa wa sasa kwa muhula mwengine hadi rais Ruto amalize zamu yake.
Kuhusu chama Salasya alisema hilo ni swala la baadaye ila akahoji uwezekano wa kujiunga na muungano wenye shabaha sawia.