Sakaja awasimamisha kazi maafisa 2 juu ya utupaji taka

Martin Mwanje
2 Min Read
Johnson Sakaja - Gavana wa Nairobi

Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja amewasimamisha kazi maafisa wawili waandamizi wa kaunti hiyo kufuatia kisa cha utupaji taka nje ya jengo la Stima Plaza la kampuni ya umeme nchini ya Kenya Power .

Akizungumza leo Jumatatu alipofika mbele ya Kamati ya Utawala na Usalama wa Ndani katika jengo la County Hall, Sakaja alilaani tukio hilo akisema lilikiuka sera na maadili ya kaunti ya Nairobi.

“Maafisa wawili wamesimamishwa kazi kuhusiana na utupaji taka kinyume cha sheria kwa sababu hiki si kile tunachokisimamia. Kwa niaba ya wafanyakazi, naomba msamaha. Hilo halikupaswa kutokea,” alisema Sakaja.

Maafisa hao, ambao hawakutajwa kwa majina, wanadaiwa kuagiza utupaji taka huo.

Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja amethibitsha kuwa uchunguzi wa jinai ulianzishwa mara moja baada ya kutokea kwa kisa hicho.

“Nilikuwa nchini Nigeria wakati huo, lakini tulianzisha uchunguzi mara moja baada ya kuripotiwa kwa utupaji taka huo kinyume cha sheria,” alisema Kanja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin amethibitisha kuwa maafisa wa Kenya Power waliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Parklands punde kilipotokea.

“Tulianzisha uchunguzi kufuatia ripoti katika kituo cha polisi cha Parklands na watu kadhaa wamekamatwa ili kuhojiwa,” alisema Amin.

Wiki jana, kulikuwa na mivutano kati ya serikali ya kaunti ya Nairobi na kampuni ya Kenya Power, kitovu cha mivutano hiyo kikiwa madai ya kutolipwa kwa madeni.

Huku serikali ya kaunti ya Nairobi ikisema inaidai Kenya Power shilingi bilioni 4 na ushei, Kenya Power ilisema inaidai serikali hiyo shilingi bilioni 3 na ushei katika kile kilichogeuka kuwa mchezo wa paka na panya.

Kiasi kwamba serikali ya Nairobi iliazimia kumwaga taka nje ya jengo la Stima Plaza wakati Kenya Power nayo ikiripotiwa kuikatia serikali hiyo umeme.

Share This Article