Sakaja atetea hatua ya kuhamisha akaunti za hospitali hadi benki ya Sidian

Marion Bosire
2 Min Read
Gavana wa Nairobi Johnson sakaja.

Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja ametetea uamuzi wake wa kuhamisha akaunti za amana za hospitali hadi Benki ya Sidian, akisema benki hiyo inatoa viwango bora kuliko benki nyingine.

Kiongozi huyo alikuwa akizungumza mbele ya Kamati ya bunge la Seneti kuhusu Ugatuzi ambapo alisema pia kwamba serikali ya kaunti ya Nairobi inazingatia kuhamisha akaunti zake zote hadi Benki hiyo ya Sidian.

Sakaja alitetea hatua hiyo akisisitiza kwamba hakuna sheria iliyokiukwa katika mabadiliko hayo ambayo yalichochewa na sababu za kiutawala na kifedha.

Kamati hiyo ya Ugatuzi ya Seneti ilikuwa imemwalika Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kujibu maswali kuhusu matumizi ya raslimali zilizotengewa maendeleo kwenye bajeti na miradi ya maendeleo iliyokwama katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023.

Gavana alitumia fursa hiyo kueleza madhumuni ya kuhamisha akaunti zote za amana za hospitali kutoka Benki ya Cooperative hadi Benki ya Sidian akisema lengo ni kuboresha ufanisi wa kifedha, kwani hapo awali kaunti ilikuwa imeathiriwa na ucheleweshaji wa benki.

Aliwafahamisha maseneta pia kuwa madeni ambayo kaunti ya Nairobi inadaiwa yamepungua kwa shilingi bilioni 32 huku mapato ya ndani yakiongezeka hadi shilingi bilioni 13.8.

Hata hivyo, Gavana Sakaja alikosoa kile alichokitaja kuwa mfumo usio na uwiano wa ufadhili wa barabara kitaifa ambapo kaunti hupokea ni shilingi bilioni 3 pekee kati ya shilingi bilioni 119 zinazotengwa kitaifa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara licha ya kusimamia asilimia 70 ya mtandao wa barabara.

Kikao cha leo cha kamati hiyo ya Ugatuzi ya Seneti na Gavana Johnson Sakaja pia kilimpa fursa Gavana huyo kuangazia masuala kadhaa yanayosibu wakazi wa Nairobi kama vile ada ya umeme wanayotozwa.

Kulingana na Sakaja, wakazi wa Nairobi hawafai kutozwa ada ya uwekaji stima mashinani akipendekeza pesa zinazokusanywa Nairobi zielekezwe kwenye mipango kama uwekaji wa taa za barabarani na vifaa vingine vya usalama.

Share This Article