Raila Odinga alizaliwa katika eneo la Maseno, kaunti ya Kisumu Januari 7, 1945, akiwa mwana wa Makamu wa Rais wa kwanza Jaramogi Oginga Odinga.
Alianza masomo katika shule ya msingi ya Kisumu Union, kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Maranda. Baadaye aliendeleza masomo yake katika taasisi ya Herder nchini Ujerumani. Odinga alihitimu na shahada ya uzamili katika sayansi ya Uhandisi mwaka 1970.
Odinga ambaye anajulikana kama Baba nchini Kenya, alijitosa katika ulingo wa kisiasa mwaka 1970, akipigia debe mabadiliko serikalini.
Ni katika harakati zake za kupendekeza marekebisho serikali, ndipo alitofautiana na Rais Daniel Arap Moi wakati huo, huku akishtumiwa kwa kujaribu kuipindua serikali mwaka 1982.
Odinga aliwekwa kizuizini kwa miaka sita baada ya kutuhumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi mwaka 1982, na baadaye alikamatwa tena kwa kushinikiza demokrasia chini ya utawala wa chama kimoja.
Baada ya kuachiliwa huru, Raila alitoroka nchini Kenya, huku akihofia kukamatwa tena.
Alirejea nchini Kenya mwezi Februari mwaka 1992 kutoka uhamishoni baada ya kuanzishwa tena kwa siasa za vyama vingi. Alijiunga na chama cha FORD.
Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 1992, Raila alichaguliwa mbunge wa eneo la Lang’ata kwa tiketi cha chama cha FORD-Kenya.
Raila aligombea urais mara tano nchini Kenya, kila wakati akiwa na chama kipya au muungano tofauti wa kisiasa. Hata hivyo, hakufua dafu katika azma yake ya kuwa Rais.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2002, Raila kupitia chama cha Liberal Democratic Party (LDP), aliungana na Mwai Kibaki aliyekuwa akiongoza chama cha National Alliance Party of Kenya (NAK) pamoja na vyama vingine na kushinda uchaguzi huo.
Wakati wa Uchaguzi wa mwaka 2013, Raila alishindwa na Uhuru Kenyatta na mwaka 2022 akabwagwa na Rais William Ruto.