Safari za ndege Zaidi ya 1,400 kwenda, kutoka au ndani ya Marekani zilifutiliwa mbali jana Jumamosi baada ya mashirika ya ndege kuagizwa wiki hii kupunguza idadi ya safari kutokana na kufungwa kwa shughuli za serikali kuu kufuatia ukosefu wa pesa.
Takribani safari 6,000 za ndege pia zilicheleweshwa, idadi ambayo imeshuka kutoka zaidi ya safari 7,000 zilizocheleweshwa Ijumaa, kwa mujibu wa tovuti ya ufuatiliaji wa safari za ndege.
Mamlaka ya Shirikisho la Usafiri wa Anga ilitangaza mapema wiki hii kwamba ingepunguza uwezo wa safari za anga kwa hadi asilimia 10 katika viwanja 40 vya ndege vilivyo na shughuli nyingi zaidi nchini humo.
Wasimamizi wa usafiri wa angani wanaofanya kazi bila malipo wakati wa kufungwa kwa shughuli za serikali wameripoti kuchoka.
Wanachama wa Republican na wale wa Democratic bado wamegawanyika kuhusu jinsi ya kukomesha mkwamo huo bungeni huku shughuli za serikali zikiendelea kusitishwa tangu Oktoba Mosi, 2025.
Maseneta wako Washington kwa mazungumzo ya pande mbili yenye lengo la kumaliza kufungwa kwa serikali, ambako sasa kumeanza kuwaathiri Wamarekani wengi zaidi kutokana na kupunguzwa kwa malipo ya misaada ya chakula na usumbufu wa safari za ndege.
Kampuni ya usafiri wa ndege ya American Airlines ilitoa taarifa jana ikiwataka viongozi kuafikia makubaliano haraka na kumaliza mkwamo wa shughuli za serikali ili kuondolea wasafiri madhila.
Uwanja wa ndege wa Newark Liberty huko New Jersey ndio ulikumbwa na muda mrefu zaidi wa wasafiri kusubiri safari zao, muda uliofikia saa nne huku kiwango wastani cha muda wa uchelewaji wa safari za ndege kikiwa saa moja unusu.