Rwanda na DRC zaafikia mkataba wa kiuchumi

Dismas Otuke
2 Min Read

Mataifa ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – DRC yametia saini makubaliano ya ya ushirikiano wa kiuchumi chini ya uongozi na uangalizi wa Marekani.

Nchi hizo zilikubaliana kuhusu mpango wa ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda ambao umepatiwa jina la ‘Washington Accord’ ambao uliafikiwa kupitia ushawishi wa Marekani.

Hatua hii ya kihistoria inalenga kuhakikisha amani na maendeleo kupitia ushirikiano wa kibiashara na miundombinu, kwa lengo la pamoja la nchi hizo kurekebisha sekta kadhaa muhimu.

Kulingana na mkataba huo, nchi hizo zitashirikiana kwa kugawana rasilimali za madini, kujenga miundombinu ya usafiri na mradi mkubwa wa nishati ya umeme wa gharama ya dola milioni 760.

Tukio hili linalenga kuvutia uwekezaji wa Magharibi huku usalama ukiboreshwa.

Tamko la pamoja lilitolewa mwisho wa kikao cha nne cha Kamati ya Pamoja ya Ufuatiliaji wa Mkataba wa Amani kati ya DRC na Rwanda, kikao ambacho kilihudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu kutoka pande zote mbili na wasimamizi wa kimataifa.

Katika taarifa hiyo ya pamoja, pande zote mbili zilikubaliana kuchukua hatua madhubuti za muda mfupi, kulingana na wajibu wao wa kimkataba, kwa ajili ya kudhibiti kundi la Waasi la FDLR na washirika wake.

Mataifa hayo yameafikiana pia kuharakisha hatua za kuondoa vikosi na kuondolewa kwa hatua za ulinzi zilizowekwa na Rwanda.

Wadadisi wanaona makubaliano haya kama hatua ya matumaini kwa eneo la Maziwa Makuu, ambalo kwa muda mrefu limegubikwa na mizozo ya kisiasa na kijeshi.

TAGGED:
Share This Article