Kila mtu katika jamii ana jukumu la kutekeleza katika kuhakikisha Kenya inafikia upeo wa maendeleo.
Ni kwa misingi hii ndiposa Rais William Ruto amesema anafanya kazi kwa karibu na viongozi wa kidini kuboresha maadili ya taifa na sekta mbalimbali kwa manufaa ya raia.
“Mabadiliko ya nchi yetu yanahitaji mtazamo wa jamii yote kwa jumla. Kila sekta, zikiwemo taasisi za kidini, zina wajibu muhimu wa kutekeleza katika kuangazia changamoto zinazoikumba nchi yetu,” alisema Rais Ruto.
“Tunafanya kazi na viongozi wa kidini kuimarisha maadili yetu ya jamii, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya na elimu bora kwa wote.”

Kiongozi wa nchi aliyasema hayo leo Alhamisi asubuhi alipokutana na maafisa wa Dayosisi ya Nairobi ya kanisa la Kiangilikana wakiongozwa na Askofu Jonathan Kabiru katika Ikulu ya Nairobi.