Serikali imezindua mpango wa shilingi trilioni tano ili kuwekeza kwa wananchi, kuimarisha kilimo kupitia unyunyuziaji mkubwa wa mashamba maji, kujenga barabara bora na mifumo ya nishati, na kufungua fursa halisi kote nchini.
Rais William Ruto alisema hayo jana Jumapili jioni alipomkaribisha Waziri Mkuu wa Malaysia Dato’ Seri Anwar Ibrahim kwa chakula cha jioni katika Ikulu ya Nairobi.
Kiongozi wa taifa alisema Kenya ilikuwa ikiiga msukumo wa Malaysia ambayo imepanda hadhi kutoka taifa linalokua hadi nchi iliyoimarika kiuchumi.
“Safari ya Malaysia inazidi kutuchochea na kudhihirisha kuwa nidhamu, mwelekeo na uongozi wenye ujasiri unaweza kubadilisha nchi,” alisema Rais Ruto.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Malaysia alipongeza mpango wa nyumba za bei nafuu nchini akisema nchi hiyo inaongoza katika kutoa nyumba nzuri kwa familia zenye kipato cha chini.
Ibrahim aliwasili nchini jana Jumapili jioni kwa ziara rasmi humu nchini kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Kuala Lumpur na Nairobi, hasa kwa kuzingatia uchumi wa kidijitali, nyumba na elimu.